Mkurugenzi wa muziki: John Kitime

Uncategorized Comments (0)

char-kitime

“Kutoka kwenye utunzi wa nyimbo kwenye simu ya mkononi…nyimbo zinazotoa simulizi zimetokea…”

Wakati Mtayarishaji katika Shirika la Kimataifa la Habari kwa ajili ya Maendeleo (MFDI), John Riber, alipokuwa anatafuta mwanamuziki wa kuboresha na kunogesha simulizi za Kumekucha, igizo la redioni, alipata mtu anayefaa kabisa, John Kitime.

Kwa Kitime, muziki upo damuni. Ubunifu wake katika utunzi wa nyimbo na ujuzi wa muziki wa asili wa Kitanzania, unaipeleka Kumekucha katika hatua nyingine.

Kitime ana namna ya pekee ya kutoa wasifu wake na kuuelezea muziki wake:

“Naitwa John F. Kitime; unaweza pia kuniita JFK. Nafikiri nimezaliwa nikiwa mwanamuziki; baba yangu alikuwa anacheza ala mbali-mbali za muziki na daima kulikuwa na muziki wakati ni mdogo. Nilipata msisiko wa kuwa jukwaani kwa mara ya kwanza nikiwa na miaka 10, kwenye mashindano ya kuimba ambapo niliimba wimbo uitwao Jamaican Farewell wa Harry Belafonte, na ni baada ya kufundishwa wimbo huu na baba yangu kwa ajili tu ya mashindano, nilishinda! Zawadi ilikuwa ni pakiti la peremende (pipi). Kwa sasa, nipo kwenye bendi ya Kilimanjaro.

Mtu ambaye alivumbua simu ya mkononi inayoweza kurekodi lazima alikuwa anakula samaki wengi. Kule ninapotoka tunaamini kwamba kula samaki wengi kunakufanya uwe na akili. Kila ninapopata wazo la tuni, ninachukua simu yangu na kurekodi tuni hiyo haraka. Nimefakiwa kupata mawazo mengi ya nyimbo, ambayo nimeyahifadhi kwenye maktaba yangu.

Nilivyoitwa ili kutunga muziki kwa ajili ya Kumekucha nilitumia nusu ya usiku kusikiliza mawazo niliyoyahifadhi kwa kipindi cha nyuma, baadhi yalikuwa hayana mpangilio au yenye ukali mpaka sikuamini kama ni mimi ndiye niliyerekodi tuni hizo za kustaajabisha. Kisha, nilipata mawazo ya kuanzia kwa ajili ya nyimbo.

Baada ya kurekodi nyimbo za msingi, ilikuwa ni muda wa kuleta wasanii ambao nilijua ni wazuri ili tuangalie tutakachoweza kufanya na mawazo yale ya nyimbo. Sikuwahi kufanya kazi na wengi wa wasanii hawa, kasoro rafiki yangu Anania Ngoliga, ambaye ni mcheza Kalimba. Tumesafiri kwenda nchi nyingi tukifanya maonyesho ya muziki wa aina yetu wenyewe, akustika ya Kalimba kwa gita la akustika, na kuna siku moja katika faraguzi la muziki jijini Mumbai, tulicheza ala za muziki za kihindi ziitwazo sitar na tablas kwenye onyesho letu. Aisee! Ilikuwa nzuri sana.

Lakini turudi studio… jambo la kufurahisha lilikuwa ni kuona ukuaji wa wazo kutoka kwenye rekodi ya simu ya mkononi kwenda katika nyimbo zenye hisia, nyimbo za huzuni, nyimbo za furaha, zote zikiwa katika muundo mpya, na zikisimulia hadithi ya Kumekucha.

Nashukuru Mungu kuna muziki.”

» Uncategorized » Mkurugenzi wa muziki: John Kitime
On June 26, 2016
By

Comments are closed.

« »